Mamia wafariki katika mkanyagano Saudi Arabia

Mamia wafariki katika mkanyagano Saudi Arabia

Eid al-Adha

Image copyrightSaudi Civil Defence Directorate
Image captionWatu zaidi ya 717 waliokuwa wakishiriki sherehe za hija wamefariki kwenye mkanyagano uliotokea karibu na mji mtakatifu wa Kiislamu wa Mecca, maafisa nchini Saudi Arabia wamesema.
Idara ya ulinzi wa raia nchini humo imesema watu wengine 863 wamejeruhiwa katika kisa hicho kilichotokea eneo la Mina, takriban kilomita tano kutoka mji wa Mecca.
Maafa hayo yalitokea mahujaji takriban milioni mbili walipokuwa wakishiriki moja ya kaida muhimu za mwisho katika ibada za hija.
Ndio mkasa mbaya zaidi kutokea wakati wa hija katika kipindi cha miaka 25.
Mahujaji husafiri hadi Mina wakati wa kuhiji kurusha mawe saba kwenye nguzo saba zijulikanazo kama Jamarat, ambazo huwakilisha shetani.
Nguzo hizo zimo katika eneo ambalo inaaminika Nabii Ibrahim alijaribiwa na shetani.
Ramani ya eneo la Mecca
Watu walikuwa wakielekea eneo la kurushia mawe, na wengine wakitokea huko pale ghafla watu walipoanza kuanguka.
Kulikuwa na raia wa Nigeria, Niger, Chad na Senegal miongoni mwa mataifa mengine.
Idara ya ulinzi wa raia Saudi Arabia imesema mkanyagano huo ulitokea pale kulipotokea "ongezeko la ghafla" la watu waliokuwa wakielekea kwenye kwenye nguzo za kurushiwa mawe.
Waziri wa afya wa Saudi Arabia Khaled al-Falih amesema mkanyagano huo ulitokea kwa sababu mahujaji walikosa kufuata maagizo.
"Wengi wa wahamiaji huenda bila kufuata ratiba iliyowekwa," amesema.
Mwandishi wa BBC Hausa Tchima Illa Issoufou aliyekuwa ameenda kuhiji ni mmoja wa walioathirika. Anasema shangazi yake alifariki na baadhi ya watu alioandamana nao hawajulikani waliko.
"Watu walikuwa tu wakiimba jina la Allah, huku wengine wakilia, wakiwemo watoto. Watu walianguka sakafuni na hakukuwa na wa kuwasaidia. Ni kana kwamba kila mtu alikuwa anajijali mwenyewe," amesema.
Mkanyagano huo umetokea siku ya kwanza ya sherehe za Eid al-Adha.
Idara ya ulinzi wa raia Saudi Arabia imesema maafisa 4,000 wametumwa eneo hilo kusaidia pamoja na wahudumu 200 wa huduma za dharura.
Kurusha maweImage copyrightAP
Image captionMahujaji hukusanyika kurushia mnara mawe kama ishara ya kumrushia shetani mawe
Maandalizi ya ibada hizo za hija yalikuwa yamekumbwa na mkasa baada ya kreni kuanguka katika msikiti mkuu wa Mecca mwezi huu na kuua watu 109.
Hii si mara ya kwanza kwa mikasa kutokea wakati wa hija.
Mikasa mingine iliyotokea wakati wa kuhiji:
2006: Mahujaji 364 walifariki wakati wa kurushia mawe mnara unaoashiria shetani
1997: Mahujaji 343 walifariki na 1,500 kujeruhiwa kwenye mkasa wa moto
1994: 270 waliuawa katika mkanyagano
1990: Mahujaji 1,426 waliuawa katika mkanyagano njia za kupitia chini za kuelekea maeneo matakatifu
1987: Watu 400 walifariki maafisa wa serikali walipokabiliana na waandamanaji waliounga mkono Iran.
Habari na picha kwa hisani ya BBCswahili