09/25/15

Nipeni mwaka mmoja tu muone mabadiliko Kinondoni!- Karama (Kalapina) Masoud

Mgombea ubunge wa jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Bw Karama Masoud aka Kalapina akiwahutubia wakazi wa Kinondoni Moscow kituo cha polisi jijini Dar es Salam leo jioni.
Msanii maarufu wa muziki wa kufoka foka nchini Bw Karama Masoud (Kalapina) leo hii aliendelea na kampeni zake za kutafuta kura katika jimbo la Kinondoni ambapo leo alifanya mkutano Kinondoni Moscow kituo cha polisi mkutano ambao ulihudhuriwa na wagombea udiwani wa kata za Ndugumbi, Magomeni, Mzimuni na Kigogo.



Awali wasanii wa muziki wa kizazi kipya Domokaya, TID, KR Mullah wa TMK Family walitoa burudani safi kwa wakazi wa eneo hilo waliohudhuria mkutano huo wa kampeni. Hata hivyo katika hali ya kustaajabisha ilitokea sintofahamu katika mkutano huo baada ya generator mbili kushindwa kufanya kazi na kuufanya mkutano huo kusimama kwa muda, ambapo ilifuatwa generator nyingine ya tatu ambayo nayo ilichukua muda mpaka ilipoweza kufanya kazi. 

Akiongea kwa hisia kali na wapiga kura hao, Kalapina alisema "Nikiwa mzaliwa na niliyekulia Kinondoni naelewa matatizo yenu kuanzia mazingira machafu, mafuriko ya mara kwa mara na gonjwa hatari la kipindupindu  na mengineyo mkinipa kura za kuniwezesha kwenda bungeni nitahakikisha katika kipindi cha mwaka mmoja tu mtaona mabadiliko ya mazingira hapa Kinondoni na ninawaruhusu nisipotekeleza mje mnifanyie fujo nyumbani kwangu na hata polisi wakija nitawaambia wananchi wangu wana haki ya kufanya wafanyalo kwa kuwa sijatimiza ahadi zangu.

Akimuelezea mbunge aliyepo sasa Mh Idi Azan alisema "Kwa miaka 10 sasa hali ya mazingira ya Kinondoni imedorora, Idi Azan hana lolote alifanyalo yani yupo yupo tu" aliongeza kusema "Kama kuna mtu yupo hapa alipata kumsikia Idi Azan akiongea chochote aje hapa aniambie nitampa sh elfu 10, jambo ambalo lilizua kelele za watu wakisema hawajawahi kumsikia akiongea chichote bungeni"
  

Baadhi ya wakazi wa Kinondoni Moscow wakimsikiliza mgombea ubunge wa jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Bw Kalapina leo jioni.
Mbgombea ubunge wa viti maalum kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Bi Asma (mwenye kilemba cha zambarau) akifuatilia hotuba mbali mbali mbali katika mkutano wa kampeni ya ubunge leo.
Mkurugenzi wa uchaguzi wa chama cha ACT Bw Nixon Tugara akihutubia wakazi wa Kinondoni Moscow
Mgombea ubunge wa viti maalum kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Bi Asma akiwasalim wakazi wa Kinondoni Moscow waliojitokeza kumsikiliza mgombea ubunge wa jimbo hilo Bw Karama Masoud. 

Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Q Chillah (fulana nyeupe) na TID (mwenye miwani na balaghashia) wakifuatilia mkutano baada ya kufanya maonesho kabla ya mkutano huo kuanza.
Baaadhi wa wafuasi wa Bw Kalapina ambaye ni mgombea ubunge wa jimbo la Kinondoni wakifuatilia mkutano.
Wagombea udiwani kwa tiketi ya ACT Wazalendo wa kata za Ndugumbi, Mzimuni, Kigogo na Magomeni wakitambulishwa kwa wapiga kura wa Kinondoni Moscow.
Mshabiki wa mgombea wa ACT Wazalendo ubunge wa jimbo la Kinondoni akishangilia huku akiwa kabeba bango lenye picha ya mgombea huyo.

Mgombea wa udiwani kata ya Hananasif wa ACT Wazalendo Bw Baruani aka Komandoo akiwasalim wapiga kura wake.







Mkurugenzi wa uchaguzi wa chama cha ACT wazalendo Bw Nixon Tugara kulia na Bi Asma wakiwa jukwaani


Mgombea wa ubunge kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo Bw Karama Masoud Kalapina katikati akifuatilia mkutano huo wa kampeni.
Bi Asma akimtambulisha Kalapina kwa wapiga kura wa Kinondoni Moscow kituo cha polisi.

Kalapina akimwaga sera makini
Picha na habari na Mkala Fundikira