December 2016

BODI YA FILAMU NCHINI YAWATAKA WADAU KUFIKISHA MISWADA YA FILAMU KUKAGULIWA KABLA YA KUIGIZWA.

Bi.Deograsia Ndunguru ambaye ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Sanaa na Habari, Chuo Kikuu Dodoma UDOM, hii leo akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya siku tatu kwa wanatasnia wa filamu na maigizo mkoani Mara, yaliyoanza jana ukumbi wa shule ya Sekondari Mara. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Bodi ya Filamu nchini.

#BMGHabari

Mtendaji Mkuu Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, Dkt.Herbert Makoye, hi leo akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya siku tatu kwa wanatasnia wa filamu na maigizo mkoani Mara, yaliyoanza jana ukumbi wa shule ya Sekondari Mara.
Wanatasnia wa filamu na maigizo mkoani Mara wakifuatilia mada kutoka kwa Mtendaji Mkuu Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, Dkt.Herbert Makoye.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu nchini, Bi.Joyce Fissoo (kushoto), akizungumza wakati wa mafunzo hayo. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo jana. Baada ya ufunguzi alishiriki na wadau wengine mafunzo hayo.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akizungumza kwenye mafunzo kwa wadau wa filamu na maigizo mkoani Mara, hii leo. Kutoka kushoto ni Mtendaji Mkuu Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, Dkt.Herbert Makoye, Bi.Deograsia Ndunguru ambaye ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Sanaa na Habari, Chuo Kikuu Dodoma UDOM na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu nchini, Bi.Joyce Fissoo
Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Simon Mwakifwamba (kuhoto) akiwa pamoja na Afisa Utamaduni Halmashauri ya Musoma Vijijini, Twalib Kamugisha (kulia) wakifuatilia mafunzo kwa wanatasnia wa filamu na maigizo mkoani Mara.
Afisa Utamaduni Halmashauri ya Musoma Vijijini, Twalib Kamugisha (kushoto) akiwa pamoja na Katibu wa Chama cha Waigizaji mkoani Mara TDFAA, Johnson Ibambai maarufu kama Dunia (kulia), wakifuatilia mafunzo kwa wanatasnia wa filamu na maigizo mkoani Mara
Wanatasnia wa filamu na maigizo mkoani Mara, wakiwa kwenye mafunzo ya filamu yanayotolewa na Bodi ya Filamu mkoani humo.
Bodi ya Filamu nchini imewataka wadau wa sekta hiyo kuwasilisha miswada ya kazi zao ili kukaguliwa kabla ya kuanza kuigiza ili kuondoa na usumbufu wa kuzifungia kazi zisizo na maadili.

Katibu Mtendaji wa bodi hiyo, Joyce Fissoo, ametoa kauli hiyo kwenye mafunzo ya siku tatu kwa wanatasnia ya filamu mkoani Mara, yanayofanyika Mjini Musoma.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuondoa usumbufu wa ambao umekuwa ukijitokeza kwa baadhi ya miswada ya filamu kurekodiwa kabla ya kukaguliwa na baadaye filamu zake kuzuiliwa wakati wa kuingia sokoni hivyo kuibua usumbufu mkubwa.

Wakiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo, Dkt.Herbert Makoye kutoka Taasisi ya Sanaa Bagamoyo pamoja na Deograsia Ndunguru kutoka Chuo Kikuu Dodoma, wamewahimiza wanatasnia wa filamu kuzingatia weledi katika uandaaji wa kazi zao kwa kuzingatia maudhui bora pamoja na maandalizi yanayokidhi uhitaji.

Washiriki wa mafunzo hayo wameelezea umuhimu wake ambapo wamesema yatawasaidia kuboresha uzalishaji wa kazi zao ikiwemo kuzingatia maudhui bora tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Bonyeza HAPA kujua zaidi

MTOTO AWAKIMBIA WAZAZI WAKE JIJINI DAR ES SALAAM KUKWEPA KUKEKETWA


Kamanda wa Polisi Ilala, Salum Hamdun


Na Dotto Mwaibale

MTOTO mwenye  umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kivule Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam jina lake linahifadhiwa ameelezea jinsi alivyofanikiwa kuwatoroka wazazi wake ili asikeketwe.

Mtoto huyo hivi sasa analelewa na msamaria mwema baada kufungua kesi  Kituo cha Polisi cha Stakishari Ukonga kufuatia kufikishwa kituoni hapo kwa ajili ya kujisalimisha na kuelezea madhila aliyotaka kufanyiwa.

Wakati mtoto huyo akijisalimisha katika kituo hicho kuna taarifa za ndani kuwa kuna mpango wa  kuwakeketa watoto  85 wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 15 katika manispaa hiyo ambapo watoto zaidi ya 30 wanadaiwa kukeketwa.

Akizungumza na mtandao wa www.habari za jamii.com mtoto huyo alisema hawezi kurudi tena nyumbani kwao kwa kuhofia kupigwa na kukeketwa ambapo ameomba msaada wa hifadhi kutoka kwa watanzania.

"Baada ya baba yangu kufariki nyumbani kwetu Tarime tulikuja na mama hapa Dar es Salaam kwa kaka yake Chacha Nyanchiri anayeishi Kitunda Kivule karibu na Shule ya Msingi Misitu" alisema mtoto huyo.

Alisema katikati ya wiki iliyopita alifika bibi yake mzaa baba yake aliyemtaja kwa jina la Boke na kuwaambia yeye na wenzake wajiandaa kwenda kukeketwa.

Mtoto huyo alisema kwamba siku ya alhamisi majira ya saa mbili usiku wakiwa nyumbani kwa mjomba wao anakoishi na mama yake alifika bibi mzaa mama yake aliyemtaja kwa jina moja la Debora huku akiwa ameongozana na mama yake Happyness na kuwaambia yeye na watoto wengine wawili wa mama yake mkubwa wakaoge ili waende kukeketwa.

Alisema ili kukwepa kukeketwa alipokwenda bafuni alifanikiwa kutoka na kupita njia nyingine na kufanikiwa kuwatoroka wazazi wake na kwenda kujificha kwenye pagala na ilipofika saa tatu usiku alifika eneo la kwa Mpemba akielekea darajani ambapo alikutana na dada mmoja aliyemsimulia mkasa huo.

Alisema dada huyo alimchukua hadi nyumbani kwake ambako alilala na siku iliyofuata alimpeleka kituo cha Polisi cha Stakishari kwa ajili ya usalama wake.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye alikataa kutaja jina lake alisema kuna mpango wa kuwakeketa watoto 85 kabla ya kuisha kwa mwaka huu wa 2016 na kuwa karibu watoto 30   wamekwisha keketwa.

Alisema shughuli hiyo inasimamiwa na wazee wa kimila wa kabila la kikurya na kuwa ngariba mkuu wa kazi hiyo ya kukeketa watoto hao yupo eneo la Nyamuhanga na kuwa baada ya kukeketwa ufanyiwa sherehe kwa siri katika baadhi ya nyumba zilizopo jirani na ngariba huyo.

Mwenyekiti wa Serikali wa mtaa anaoishi mtoto huyo, Dominick Mlimi alisema hana taarifa ya mtoto huyo kutoweka nyumbani kwao.

"Jana niliwaona baadhi ya watoto wa kike wa familia ya Nyanchiri wakiwa hapo barabarani lakini kuhusu kutoweka kwa mtoto huyo kwa kuhifia kukeketwa sijazipata" alisema Mlimi.

Mke wa Chacha Nyanchiri ambaye anaishi na mtoto huyo Regina Wilison alikiri mtoto huyo kuondoka  usiku baada ya kufika nyumbani hapo bibi yake na mama yake ingawa alisema hawakutoa taarifa kwa mtu yeyote ya kutoweka kwake.

"Mwenye mamlaka ya mtoto huyo ni mama yake ambaye ametoka asubuhi kwenda kumtafuta mtaani mimi sihusiki naye na wala sijui walichomuambia ingawa siku zote tulipokuwa tukizungumzia kuhusu kukeketwa mtoto huyo alikuwa akionesha hofu" alisema Wilison.

Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamdun alisema hakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo ingawa aliahidi kuwasiliana na wasaidizi wake ili kulifuatilia na kutoa taarifa kamili.

Mtoto huo alisema watoto wenzake waliofanyiwa vitendo hivyo bado wapo majumbani mwao wakijiuguza majeraha na kama vyombo vya usalama vitahitaji kwenda kuwaonyesha walipo yupo tayari. 

Taarifa ambazo tumezipata jana kutoka kwa baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na nyumba aliyokuwa akiishi mtoto huyo na mama yake zimeeleza kuwa polisi walifika katika nyumba hiyo na kumkamata Regina Wilson, mama ya mtoto huyo Happyness na watu wengine wawili na kupelekwa kituo cha polisi Stakishari Ukonga jijini Dar es Salaam kwa mahojiano.


SUALA LA UKEKETAJI MKOANI MARA BADO NI PASUA KICHWA.

>
Baadhi ya wasichana wakitoka kukeketwa wilayani Tarime mkoani Mara, kumbuka mwezi Disemba, kila baada ya miaka miwili, ni msimu wa ukeketaji na tohara kwa baadhi ya Koo za Wakurya 
  
BMGHabari

Pamoja na juhudi za Serikali, Wanaharakati na Watetezi wa haki za binadamu (Wanawake na Wasichana) katika kuhakikisha kwamba suala la ukeketaji linatokomezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Mara na Arusha, bado suala hilo ni pasua kichwa kwani linafanyika, iwe kwa uwazi ama usiri.

Mtandao wa Binagi Media Group umeshuhudia baadhi ya wakazi wa wilaya ya Tarime wakisherehekea msimu huu wa ukeketaji (Mwezi Disemba kwa baadhi ya koo, ikiwemo Watimbaru) ambapo wasichana wadogo wanafanyiwa ukeketaji.

Shamra shamra zinafanyika hadharani licha ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, kuonya kwamba yeyote atakayebainika kujihusisha na ukeketaji atachukuliwa hatua za kisheria.

Baadhi huamini kwamba msichana akikeketwa huleta heshima kwake na kwa familia na huwa tayari kwa ajili ya kuolewa na hivyo kuwapatia wazazi mahari (ng'ombe). Hatua hii husababisha baadhi ya mabinti kukosa fursa ya kuhitimu masomo yako na kujikuta wakiolewa, Aidha kwa kupenda ama kulazimishwa na wazazi/walezi wao. Suala la unyanyapaa miongoni mwa wasichana waliokeketwa na ambayo hawajakeketwa ni jambo ambalo pia huongeza msukumo wa wasichana kutaka kukeketwa. Mbaya zaidi, unyanyapaa huo huenda hadi kwa baadhi ya wanaume kukataa kuwaoa wale ambao hawajakeketwa na hivyo kusababisha ugumu wa kutokomeza suala hilo.

Tayari Ngariba mmoja aitwaye Angelina ppCharles (50) amehukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezaji kwa kosa la kumfanyia ukeketaji mmoja wa wasichana wilayani humo huku wengine wawili wakidaiwa kukabiliwa na kesi ya aina hiyo. Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Mhe.Martha Mpaze.

Wakati hayo yakiendelea, zipo kauli mbalimbali wilayani Tarime kwamba hivi sasa wasichana hawakeketwi kama zamani bali wakifika eneo la tukio hupakwa unga kwenye uso na maumbile yao na kufanyiwa matambiko ya kimila na shughuli huishia hapo na kinachofuata ni shamra shamra za kucheza ngoma ya ritungu na kurejea nyumbani.

Hata hivyo utafiti uliofanywa mwishoni mwa mwaka jana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na idadi ya watu duniani, UNFPA, kwenye mikoa 13 nchini ikiwemo Mara, umebaini kwamba katika maeneo mengi nchini, wanajamii wanazo mbinu mpya za kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kukumbatia mila potofu ikiwemo ukeketaji. Utafiti huo ulibaini kuwa, suala la kuwapaka unga usoni wasichana wilayani Tarime ni kuuficha tu ukweli kwamba wasichana hao hawakeketwi wakati ukweli ni kwamba hukeketwa.

Itoshe tu kusema kwamba, elimu zaidi inahitajika ili kuwanusuru wasichana wanaotoka kwenye makabila yanayojihusisha na ukeketaji kwani madhara yake ni makubwa ikiwemo kupoteza damu nyingi, kupata madhara kabla na baada ya kujifungua, kupoteza uwezo wa kufurahia tendo la ndoa, uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa ikiwemo Virus vya Ukimwi na wakati mwingine kupoteza maisha.
Inaelezwa kwamba msichana anayekeketwa hulipia kiasi cha shilingi elfu 35 hadi 40 ambapo wazee wa kimila hugawana pesa hiyo na mangariba hivyo inawezekana suala hili linakuwa na ugumu kutokomezwa maana ni sehemu ya ujira kwa wazee na mangariba hao.
Inadhaniwa kwamba zaidi ya wasichana 3,000 kwa Koo moja ya kabila la Wakurya hukeketwa kwa kila msimu. Kabila la Wakurya lina Koo 13.
Wakazi wa Wilaya ya Tarime wanasema, msukumo wa ukeketaji umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Wanasema suala la elimu juu ya madhara ya ukeketaji pamoja na mwingiliano wa makabila mbalimbali ya ndani na nje ya mkoa wa Mara, umesaidia japo kwa kiasi kidogo kupunguza ari ya ukeketaji.
Kataa Ukeketaji, haina umuhimu kufurahia mila na tamaduni zenye athari katika jamii. Vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuwakama na kuwafungulia mashtaka.

Wakati haya yanaendelea, zaidi ya wasichana 250 kutoka maeneo mbalimbali mkoani Mara na Arusha, wamehifadhiwa katika kituo cha kuwahifadhi wasichana waliokimbia ukeketaji cha Masanga kilichopo wilayani Tarime.

BMG inaamini kwamba, Imani humalizwa kwa Imani. Suala la Ukeketaji ni Imani hivyo itolewe elimu yenye uhusiano wa kiimani ikiwemo maandiko matakatifu (dini) hatua ambayo itasaidia kuwanusuru wasichana wengi na suala hilo la ukeketaji.