Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo (kushoto) alipomtembelea ofisini kwake jijini Mwanza akiwa ameambatana na Mbunge wa Viti Maalum CCM, anayetetea maslahi ya watu wenye albinism, Mh. Al-Shaymaa Kwegyir (wa pili kulia) pamoja na Semeni Kingaru (wa tatu kulia).
Na Mwandishi wetu, Mwanza
SHIRIKA la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limeahidi kusaidia mapambano dhidi ya unyanyasaji na dhuluma zinazofanywa jamii dhidi ya watu wenye albinism.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues wakati akizungumza na mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo.
Mwakilishi huyo wa Unesco amesema hayo alipomtembelea Mkuu wa mkoa kumsalimia na kumweleza hatua zinazochukuliwana Unesco katika kukabiliana na ukatili dhidi ya watu wenye albinism.
Akifafanua zaidi alisema kwamba UNESCO haijatenga fedha zitakazotumika kuendesha kampeni mahsusi bali itatumia uwezo wa kiufundi uliopo kwa wataalamu walionao na kwamba wanakusudia kuona kwamba miaka 15 ijayo watoto wanaozaliwa nchini Tanzania wanakuwa huru pasipo na viashiria vya kuhatarisha maisha vinavyosababishwa na mauaji ya watu wenye albinism.
Akimkaribisha Bi Zulmira ofisini kwake, Mkuu wa mkoa Magesa Mulongo alisema kwamba ingawa kuna utulivu katika kipindi hiki mkoani Mwanza, bado mkoa wake unaendelea kukabiliana na viashiria vinavyosababisha ukatili kwa watu wenye albinism na wazee.
Bwana Magesa alisema imani potofu zilizopo zinazosadikika kufanikisha biashara za uvuvi wa samaki, uchimbaji wa madini na wanasiasa kuendelea na madaraka ni miongoni mwa sababu kubwa za mauaji hayo yaliyoitia doa jeusi jamii ya kitanzania nje ya mipaka.
Alisema kwamba jitihada zinafanywa kukabiliana na imani hizo potofu kwa kuihamasisha jamii kutoziamini na kwamba madaraka na utajiri unatokana na juhudi, kufanya kazi kwa bidii na si vinginevyo.
Aidha amesema mkoa wake umekuwa ukihakikisha kwamba makundi yanayotumika kuua watu wengine kwa kushirikisha jamii yanavunjwa na pia kuwachukulia hatua kali wote wanaobainika kushiriki kwa njia moja au nyingine.
Hata hivyo mwakilishi wa umoja wa mataifa alisema kwamba hali ya amani itatawala pale tu watu watakapobaini kwamba kuua ni ukiukwaji wa haki za binadamu na ni kosa la jinai.
Alisema pindi binadamu watakapokiri kwamba binadamu wote ni sawa na kuishi na albinism sio ‘mzimu’ watabadili mwelekeo mzima wa fikra potofu kimaisha na kuishi kwa amani na kuthaminiana.
Bi Zulmira alimwambia mkuu wa mkoa kwamba UNESCO kwa kushirikiana na wadau wengine wataendesha makongamano yenye lengo la kushirikisha jamii katika kuandaa na kutekeleza mikakati itakayo changia kuzuia na kutokomeza unyanyasaji na dhuluma zinazofanya dhidi ya watu wenye albinism.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo (kushoto) akizungumza na Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kushoto) aliyeambatana na Mbunge wa Viti Maalum CCM, anayetetea maslahi ya watu wenye albinism, Mh. Al-Shaymaa Kwegyir (wa pili kulia) pamoja na Semeni Kingaru (wa tatu kulia) alipomtembelea ofisini kwake jijini Mwanza. Wa pili kushoto ni Katibu Tawala wa mkoa wa Mwaza, Faisal Issa.
Warsha hizo zitafanyika kwa wakati tofauti katika kipindi cha wiki mbili wilayani Sengerema, Misungwi, Msalala na Bariadi. Warsha hizo zilizoanzia Sengerema Jumatano na kumalizika Ijumaa zitafuatiwa na Misungwi Mei 25 hadi 27, Msalala Mei 28 hadi 30 na Bariadi kuanzia Mei 28-30.
Katika warsha hiyo pamoja na kujadili mada mbalimbali, mijadala itahusisha viongozi wa serikali, wanasiasa, viongozi wa kidini na kimila na hoja kubwa itakayojadiliwa ni dhana ya kisayansi ya albinism, mitazamo ya jamii kuhusu dhana hiyo, makundi mbalimbali ndani ya jamii, tofauti kati ya utamaduni na asili.
Pia watajadili kubainisha na kuanisha matatizo, changamoto na hatari zinazowakabili watu wenye alibinism na kuchambua mambo yanayochangia uwepo wa changamoto na hatari kwa watu wenye alibinism.
Katika majadiliano hayo pia mikakati inayoweza kupunguza au kumaliza kabisa matatizo changamoto na hatari zinazowakabili watu wenye alibinism katika jamii yetu itatazamwa.
Watoa mada wanatarajiwa kutoka katika halmashauri, vyama vinavyotetea maslahi ya albinism, mbunge anayetetea maslahi ya watu wenye albinism Al-Shaymaa Kwegyir na mwakilishi kutoka baraza la taifa la dawa asilia.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo akiendelea na maongezi na ugeni huo ofisini kwake jijini Mwanza.
Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kulia), akielezea nia ya Shirika lake kusaidia mapambano dhidi ya unyanyasaji na dhuluma zinazofanywa jamii dhidi ya watu wenye albinism nchini alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo ofisini kwake jijini Mwanza.
Kiongozi wa ofisi na mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Zulmira Rodrigues (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo (kushoto) alipomtembelea ofisini kwake jijini Mwanza akiwa ameambatana na Mbunge wa Viti Maalum CCM, anayetetea maslahi ya watu wenye albinism, Mh. Al-Shaymaa Kwegyir (wa pili kulia) pamoja na Semeni Kingaru (wa tatu kulia).
(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog).