09/17/15

MSAFARA WA SUGU WASHAMBULIWA KWA MAWE AKIELEKEA KATIKA KAMPENI ZAKE ZA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA MBEYA


Gari la Mgombea Ubunge jimbo la Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi Sugu likiwa kituo cha Polisi kati jijini Mbeya mara baada ya kushambuliwa kwa mawe na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.
Sugu akiwa kituo cha Polisi na wafuasi wake.Picha Kenneth Ngelesi Mbeya .


Na Emanuel Kahema ,Mbeya


MGOMBEA ubunge  kupitia chadema jimbo la Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi leo  amejikuta katika wakati mgumu baada ya msafara wake kushambuliwa na mawe na wafuasi wanaosadikiwa kuwa ni wa chama   cha mapinduzi CCM na kwamba katika tukio hilo watu wawili wamejeruhiwa akiwemo dereva aliyekuwa akimuendesha mgombea huyo  .

Tukio hilo la kushambuliwa kwa msafara huo, limetokea majira ya saa 11 za jioni katika eneo  la barabarani lililopo katika Kata ya Ghana mtaa wa Mbata jijini hapa  ambapo inasemekana mgombea huyo alikuwa  katika harakati za kampeni kuomba kura kwa wananchi wa Iziwa  ambapo mgombea huyo alikuwa ndani ya gari yake yenye namba za usajili T161 CPP Toyota  Land Cruser VX .

Awali, wafuasi wa chama cha mapinduzi CCM, walikuwa katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea wao ngazi ya Udiwani katika kata ya Ghana iliyopo ndani ya Jiji la Mbeya, hivyo wakiwa kwenye harakati hizo inasemekana walishangaa kuona msafara wa sugu ukipita katikati ya mkutano huo hivyo kushindwa kuvumilia na kuanza kurusha mawe huku wengine wakishikana mithili ya kutaka kupigana.

Katika vurugu hizo gari aliyokuwa amepanda mgombea huyo  lilipasuliwa kioo cha mbele na gari ya chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Mbeya, ikipasuliwa kioo cha mbele .


Aidha Vurugu hizo zimesababisha   majeruhi wawili ambao wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya akiwemo dereva wa mbunge huyo na mfuasi mmoja wa chadema.

Kutokana na hali hiyo  mgombea huyo wa ubunge mbeya mjini kwa tiketi ya Chadema alilazimika kuikatisha zoezi lake la kuongea na wakazi wa Kata ya Iziwa iliyopo Jijini Mbeya kwa muda, kutokana na kulazimika kuripoti katika kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa maelezo.

Mgombea huyo ilimlazimu kufika kituoni na kuchukuliwa maelezo na baada ya hapo aliruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kisiasa lakini gari yake yenye namba za usajili T161 CPP aliyokuwa akiitumia katika kampeni zake ikibaki polisi.

Hata hivyo, mgombea huyo alipomaliza kutoa maelezo  katika kituo cha polisi cha kati cha Wilaya ya Mbeya, aligoma kuzungumza na vyombo vya habari ambavyo vilikuwa kwenye eneo la tukio na kuwataka wafike katika mkutano kwani ndipo atakapotolea ufafanuzi wa suala hilo hilo.

                      (JAMIIMOJABLOG MBEYA )

TAMASHA LA 34 LA KIMATAIFA LA SANAA NA UTAMADUNI KUFANYIKA TAREHE 21-27, 2015, MJINI BAGAMOYO MKOANI PWANI


 Mwenyekiti wa Tamasha la 34 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni, John Mponda (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu tamasha hilo litakalofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 27, 2015 katika Kumbi na Viunga vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), mkoani Pwani. Kulia ni Katibu wa Tamasha hilo na Ofisa Biashara, Benjamini Malimbali na Ofisa Habari, Sophia Mtakajimbo.
  Hapa Mwenyekiti wa Tamasha hilo, John Mponda (kulia) akisisitiza jambo kuhusu tamasha hilo. Kushoto ni Ofisa Habari wa Tamasha la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).
 Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.


TAMASHA la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo liliasisiwa mwaka 1981 na Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambacho kwa sasa ni Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo. Lengo kuu la Tamasha kwa wakati huo ilikuwa ni kuwapa nafasi wanafunzi wa chuo cha sanaa kuonyesha kwa vitendo yale waliojifunza kwa mwaka mzima kwa kuwashirikisha wakazi wa Bagamoyo, baada ya Tamasha hilo kufanikiwa uongozi wa chuo uliamua tamasha hilo lifanyike kila mwaka kwa kushirikisha Vikundi mbalimbali vya ndani na nje ya nchi ili kubadilishana Uzoefu  na hivyo kujizolea umaarufu ndani na nje ya Tanzania.

Tamasha la kimataifa la sanaa na utamaduni Bagamoyo mwaka huu litafanyika kwa mara ya 34 kuanzia tarehe 21-27 Septemba katika kumbi na viunga vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambao ndio wenyeji na waandaaji wa tamasha hilo kongwe Tanzania.

Maandalizi yote ya Tamasha hili yamekamilika Tamasha la mwaka huu linabeba Kauli mbiu isemayo SANAA NA UTAMADUNI KATIKA UCHAGUZI HURU NA WA AMANI’  Aidha kutakuwa na mada ndogondogo zitakazotolewa kupitia kongamano na warsha zitakazohusu  Haki za binadamu, Rushwa na kupinga Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino)

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Tamasha atakuwa mzee Rashid Masimbi, aliyekuwa mkuu wa chuo wa kwanza toka taasisi ilivyokuwa chuo cha sanaa,hivyo kwa kutambua mchango wake kwenye sanaa Taasisi imempa heshima ya kuwa mgeni rasmi .

Tamasha la mwaka huu litahusisha Ngoma za Asili, Maigizo, Sarakasi, Mazingaombwe, Muziki wa kisasa na asili, Sanaa za Ufundi  na bidhaa mbalimbali.

Jumla ya vikundi 65 kutoka ndani na nje ya Tanzania vimethibitisha kushiriki,ambapo vikundi 59  ni kutoka ndani ya Tanzania na vikundi 6 kutoka nchi za Kenya, Namibia, Afrika Kusini, Korea na Congo na Zimbabwe.

Kiingilio kwenye tamasha kwa wakubwa shilingi 3000/=,kwa watoto shiling 1000/= na kwa wageni wasio watanzania  shilingi 5000/=

Taasisi inatoa wito kwa wadau mbalimbali wa Sanaa,Makampuni,Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kujitokeza kudhamini tamasha hili muhimu ambalo hufanyika kila mwaka ili kulifanya liwe bora na la kimataifa zaidi , kwa mustakabali wa sanaa na utamaduni wa Mtanzania. 


MAGUFULI APOKELEWA KAMA MFALME KIGOMA,WANANCHI WAKIRI WAZI ATOSHA KUWA RAIS


Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kupitia chama cha Mapinduzi Dkt John Pombe Magufuli akiwahutubia  maelfu ya wananchi waliofurika kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za Urais,uliofanyika katika uwanja wa Kawawa,mkoani Kigoma jioni ya leo.

 Dkt Mafuli amewaabia wananchi wa Kigoma kwenye mkutano wa kampeni leo jioni kwenye uwanja wa kawawa kuwa Serikali yake kwa sehemu kubwa itakuwa upande wa wananchi wanyonge ili hatimaye wawe na maisha yenye neema,amesema kuwa Serikali yake haitakuwa ya kunyanyasa mama ntile na kudaiwa kodi za hovyo hovyo,amesema kuwa ataimarisha ukusanyaji wa kodi kwenye serikali yake, lakini pia atawabana wafayabiashara  wakubwa ambapo baadhi yao hawalipi kodi

Magufuli amewataka Wananchi kumuamini kwa yale ambayo amekuwa akiyasema kwenye mikutano yake ya kampeni na kuongeza anachoahidi ndicho ambacho atakitekeleza kwenye serikali yake na kwenye maisha yake huwa hataki kutoa ahadi za uongo.

 Aidha hadi jana, tarehe 16 September 2015, Mgombea Urais wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alikuwa amekwishafanya kampeni katika mikoa 12 na Majimbo 94. Amekwishafanya mikutano mikubwa ya hadhara 76 na mikutano ya barabarani 381. Amekwishatembea, kwa gari, jumla ya kilomita 13,720. Kwa ujumla amekwishakutana, moja kwa moja, na asilimia zaidi ya 30 ya wapiga kura.
Wananchi na Mabango yao
Mgombea Urais wa CCM Dkt John Pombe Magufuli akiwahutubia wakazi wa Nguruka kwenye mkutano wa kampeni wa hadhara mapema leo mchana.
Wakazi wa Nguruka waifuatilia Mkutano.
Mgombea Urais wa CCM Dkt Magufuli akimkabidhi Ilani ya chama cha CCM kwa Mgombea Ubunge wa Kigoma Kusini,Hasna Mwilima na pia kummwombea kura kwa wananchi mapema leo kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Nguruka mkoani Kigoma.
Wananchi wakisikiliza sera za Mgombea Urais wa CCM Dkt John Pombe Magufuli
Baadhi ya Wananchi wa Uvinza wakiwa wamefunga barabara wakitaka wasikilizwe kero zao na Mgombea Urais wa CCM,Dkt Magufuli alipokuwa akipita mjni humo akielekea Kigoma mjini kwenye mkutano wa hadhara.
Baadhi ya akina mama wakishangilia jambo
Mgombea Ubunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini Peter Selukamba akiwahutubia wananchi wa Kalinzi,mkoani Kigoma kwenye mkutano wa kampeni za Uraisi jioni ya leo.
Baadhi ya wafuasi wa chama cha CCM wakifuatilia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kalinzi,ambapo mgombea Urais wa CCM Dkt Magufulia aliwahutubia wananchi.
Wakazi wa mji wa Nguruka,mkoani Kigoma wakifuatilia mkutano wa hadhara
Wananchi na mabango yao
Kada maarufu na aliyewahi kuwa Katibu MKuu wa CCM,Mh Yusuph Makamba akisalimiana na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kupitia chama cha CCM Dkt John Pombe Magufuli kabla ya kupanda jukwaani na kuwaomba ridhaa wakazi wa kigoma ya kuwaongoza katika awamu ya tano.
Wananchi wakishangilia jambo kweye mkutano wa kampeni za Urais

Wananchi wakifuatilia mkutano wa kampeni
Kada maarufu na aliyewahi kuwa Katibu MKuu wa CCM,Mh Yusuph Makamba akiwahutubia wananchi wa Kigoma na vitongoji vyake jioni ya leo kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za Urais,uliofanyka katika uwanja wa Kawawa mkoani Kigoma

Picha zote na Michuzi Jr