09/24/15

Mamia wafariki katika mkanyagano Saudi Arabia

Eid al-Adha

Image copyrightSaudi Civil Defence Directorate
Image captionWatu zaidi ya 717 waliokuwa wakishiriki sherehe za hija wamefariki kwenye mkanyagano uliotokea karibu na mji mtakatifu wa Kiislamu wa Mecca, maafisa nchini Saudi Arabia wamesema.
Idara ya ulinzi wa raia nchini humo imesema watu wengine 863 wamejeruhiwa katika kisa hicho kilichotokea eneo la Mina, takriban kilomita tano kutoka mji wa Mecca.
Maafa hayo yalitokea mahujaji takriban milioni mbili walipokuwa wakishiriki moja ya kaida muhimu za mwisho katika ibada za hija.
Ndio mkasa mbaya zaidi kutokea wakati wa hija katika kipindi cha miaka 25.
Mahujaji husafiri hadi Mina wakati wa kuhiji kurusha mawe saba kwenye nguzo saba zijulikanazo kama Jamarat, ambazo huwakilisha shetani.
Nguzo hizo zimo katika eneo ambalo inaaminika Nabii Ibrahim alijaribiwa na shetani.
Ramani ya eneo la Mecca
Watu walikuwa wakielekea eneo la kurushia mawe, na wengine wakitokea huko pale ghafla watu walipoanza kuanguka.
Kulikuwa na raia wa Nigeria, Niger, Chad na Senegal miongoni mwa mataifa mengine.
Idara ya ulinzi wa raia Saudi Arabia imesema mkanyagano huo ulitokea pale kulipotokea "ongezeko la ghafla" la watu waliokuwa wakielekea kwenye kwenye nguzo za kurushiwa mawe.
Waziri wa afya wa Saudi Arabia Khaled al-Falih amesema mkanyagano huo ulitokea kwa sababu mahujaji walikosa kufuata maagizo.
"Wengi wa wahamiaji huenda bila kufuata ratiba iliyowekwa," amesema.
Mwandishi wa BBC Hausa Tchima Illa Issoufou aliyekuwa ameenda kuhiji ni mmoja wa walioathirika. Anasema shangazi yake alifariki na baadhi ya watu alioandamana nao hawajulikani waliko.
"Watu walikuwa tu wakiimba jina la Allah, huku wengine wakilia, wakiwemo watoto. Watu walianguka sakafuni na hakukuwa na wa kuwasaidia. Ni kana kwamba kila mtu alikuwa anajijali mwenyewe," amesema.
Mkanyagano huo umetokea siku ya kwanza ya sherehe za Eid al-Adha.
Idara ya ulinzi wa raia Saudi Arabia imesema maafisa 4,000 wametumwa eneo hilo kusaidia pamoja na wahudumu 200 wa huduma za dharura.
Kurusha maweImage copyrightAP
Image captionMahujaji hukusanyika kurushia mnara mawe kama ishara ya kumrushia shetani mawe
Maandalizi ya ibada hizo za hija yalikuwa yamekumbwa na mkasa baada ya kreni kuanguka katika msikiti mkuu wa Mecca mwezi huu na kuua watu 109.
Hii si mara ya kwanza kwa mikasa kutokea wakati wa hija.
Mikasa mingine iliyotokea wakati wa kuhiji:
2006: Mahujaji 364 walifariki wakati wa kurushia mawe mnara unaoashiria shetani
1997: Mahujaji 343 walifariki na 1,500 kujeruhiwa kwenye mkasa wa moto
1994: 270 waliuawa katika mkanyagano
1990: Mahujaji 1,426 waliuawa katika mkanyagano njia za kupitia chini za kuelekea maeneo matakatifu
1987: Watu 400 walifariki maafisa wa serikali walipokabiliana na waandamanaji waliounga mkono Iran.
Habari na picha kwa hisani ya BBCswahili

RAIS DK. JAKAYA KIKWETE ATOA ZAWADI YA IDD EL HAJI KWA MAKUNDI MBALIMBALI


 Kamshna Msaidizi Kitengo cha Walemavu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Beatrice Fungamo (kulia), akimkabidhi Mwakilishi wa Mahabusu ya Watoto Upanga, Regina Kuname msaada wa vyakula na kitoweo cha mbuzi na mafuta ya kula kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya ya Idd El Haji Dar es Salaam leo asubuhi.
 Kamshna Msaidizi Kitengo cha Walemavu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Beatrice Fungamo (kulia), akimkabidhi Katibu Mtendaji wa Chama cha kulea Watoto Mayatima (Chakuwama) cha Sinza, Hassan Hamisi kwa ajili ya sherehe hiyo.
 Mbuzi wakiingizwa kwenye gari baada ya wahusika kukabidhiwa.
 Vyakula vilivyotolewa na Rais Jakaya Kikwete vikiwa eneo la tukio vikisubiri kuchukuliwa.
Mwakilishi wa Kituo cha Wazee na Wasiojiweza cha Nunge kilichopo Kigamboni, David Mpangala akiwa na mbuzi waliotolewa kwa ajili ya kituo hicho.

Na Dotto Mwaibale

RAIS Jakaya Kikwete ametoa zawadi ya vyakula na kitoweo kwa makundi mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Idd El Haji ambayo inaadhimishwa duniani kote leo.

Zawadi hiyo imekabidhiwa kwa makundi hayo kwa niaba yake na Kamshna Msaidizi Kitengo cha Walemavu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Beatrice Fungamo Dar es Salaam leo asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi zawadi hiyo, Fungamo alisema Rais ametoa zawadi hiyo kwa ajili ya Sikukuu ya Idd El Haji kama anavyofanya siku zote wakati wa sikukuu mbalimbali.

Fungamo alitaja vituo vilivyopata zawadi hiyo kuwa ni Mahabusu ya Watoto ya Upanga iliyopo Manispaa ya Ilala, Makazi ya Wazee wasiojiweza ya Nunge, Kigamboni, Chuo cha Watu wenye Ulemavu cha Yombo Temeke na Kituo cha Kulelea Watoto Mayatima (Chakuwama) cha Sinza.

Alitaja vituo vingine kuwa ni Kituo cha Makao ya Watoto Yatima cha Mburahati, Ilala, Kituo cha Makao ya Watoto-Kurasini, Kituo cha Full Gospel, Temeke na Kituo cha Watoto Alsaad Children House Kurasini.

Alivitaja vituo vingine kuwa ni cha Vosa Mission cha Kongowe, Temeke na Kituo cha Kijiji cha Furaha kilichopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Fungamo alitaja vituo vilivyopata zawadi hiyo ya Idd El Haji kwa upande wa Zanzibar kuwa ni Kituo cha Mabaoni kilichopo Pemba na Makazi ya Wazee Sebleni yaliyopo Unguja.

Alitaja vituo vingine vilivyopo mikoani vilivyopata zawadi hiyo kuwa ni kituo cha The Village of Home cha Dodoma, kituo cha Moyo Mmoja cha Bagamoyo mkoani Pwani, kituo cha watoto cha Tosamaganga kilichopo mkoani Iringa na Mahabusu ya Watoto Arusha na Tanga.

SWALA YA IDD EL HAJI ILIVYOFANYIKA VIWANJA VYA MWEMBE YANGA TEMEKE JIJINI DAR ES SALAAM LEO


 Sheikh Abdu Kadri akiongoza swala ya Idd El Haji katika viwanja vya Mwembe Yanga Temeke Dar es Salaam leo asubuhi. Waislam wa Tanzania leo waliungana na wenzao duniani kote kusherehekea Sikukuu ya Idd El Haji.
 Sheikh Nurdin Kishki alipohotuba baada ya swala hiyo.
 Sheikh  Othman Dishi akitoa maelekezo kabla ya kuanza kwa swala hiyo.
 Waumini wa dini ya kiislam wakiwa katika swala.
 Wanawake na watoto wakiwa kwenye swala hiyo.
 Mazuria ya kuswalia yakitandikwa kabla ya kuanza ibada.
 Hapa wakitawaza kabla ya kuinza kwa swala hiyo.
Abdurahi Suleiman (kulia), akiuza mafuta na manukato mbalimbali katika viwanja hivyo.
 Ibada ya swala ya Idd El Haji ikiendelea.
 Biashara ya Balaghashia ikiendelea katika viwanja vyao.
 Swala ikiendelea katika viwanja hivyo.
 Pikipiki na baiskeli zikiwa zimewekwa kwa pamoja kwa ajili ya usalama.
 Mwanahabari akichukua picha katika ibada hiyo.
 Waumini wa kiislam wakiwa katika viwanja hivyo wakati wa ibada hiyo.
 Hapa salamu zikiendelea.
 Sheikh Othmani Dishi (kushoto), akisalimiana na Sheikh Abdu Kadri kabla ya kuanza kwa swala hiyo.
 Swala ikifanyika katika viwanja hivyo.
 Swala ikifanyika kwa unyenyekevu mkubwa.
Swala ikiendelea.