Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (kulia), akihutubia wananchi baada ya kupokea matembezi ya amani ya vyama vya siasa yaliyofanyika kuanzia eneo la Magomeni hadi viwanja vya Kinondoni Biafra Dar es Salaam leo asubuhi.
Mwenyekiti wa Wilaya ya Chama cha Union For Multi Party Democratic (UMD), Abdallah Tumbo akihutubia katika mkutano huo.
Katibu wa Wilaya ya Kinondoni wa Chama cha UDP, Makoye Ikoles, akizungumza katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Wilaya wa Chama cha UPDD, Salim Choya akizungumza katika mkutano huo.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kinondoni, Athuman Shesha akihutubia katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani wa dini zote Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum, akiongoza dua za kuombea nchi amani katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani wa dini zote Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni katika mkutano huo.
Dua la kuombea taifa ikiendelea.
Vijana wa Jogging wakishiriki matembezi hayo.
Matembezi yakiendelea.
DC Makonda (katikati), akiwa na Viongozi wa vyama vya siasa walioshiriki maandamano hayo.
Vijana wa Jogging wakiwa jukwaa kuu wakiimba wimbo maalumu wa amani.
Na Dotto Mwaibale
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda amesema kila mtu ana wajibu wa kuilinda na kudumisha amani iliyodumishwa na waasisi wa nchi hii hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Makonda alitoa mwito huo wakati akihutubia wananchi baada ya kupokea matembezi ya kuombea nchi amani yaliyofanyika katika viwanja vya Biafra Dar es Salaam leo.
Maandamano hayo yameratibiwa na Makonda katika wilaya yake kwa niaba ya watanzania wote.
Makonda alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizodumu kwa amani na amani hiyo ilidumishwa na waasisi wa Taifa hivyo imebaki kuwa kimbilio na tegemeo kwa watanzania.
Alisema ili kuwaenzi waasisi hao ni kutunza tunu hiyo na kwamba yapo mataifa yamepita katika nyakati mbalimbali za uchaguzi lakini hawana amani kama tuliyonayo hivyo tuna wajibu mkubwa kuitunza.
"Vipo viashiria vya uvunjifu wa amani, lakini ikumbukw kuwa amani ni kubwa kuliko ahadi za mgombea yoyote wa chama cha siasa hivyo hakuna kinachoweza kufanywa na mgombea yeyote kama hakuna amani,"alisema.
Hata hivyo Makonda alisema kuwa aliandika barua kwa kila chama cha siasa ambapo vyote vilithibitisha kushiriki lakini cha kushangaza baadhi havijahudhuria kwa kutoa sababu zisizo na msingi wowote kama kutokuwa na nauli na mambo mengine.
"Niliviandikia barua vyama vyote, lakini vingine havijahudhuria kwa makusudi hivyo dalili mnayoona hapa ni dalili tosha kuwa amani wanayohubiri kwenye majukwaa si hii wanayoitaka,"alisema Makonda.
Makonda aliongeza kuwa vyama vilivyoshiriki katika maandamano hayo ya amani ni CCM, CUF, UPDP, UDP,UMD, Jahazi asilia na vilabu vya Jogging .
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum alisema mtu yeyote asiyependa amani ni adui wa Mungu.
Sheikh Alhad aliitoa kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam leo wakati alipoongoza dua maalum ya kuombea amani wakati wa maandamano ya vyama vya siasa yaliyofanyika kuanzia eneo la Magomeni hadi viwanja vya Kinondoni Biafra.
Alisema kuwa anavipongeza vyama vilivyothibitisha kushiriki maandamano hayo pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Konondoni, Paul Makonda na kamati ya ulinzi kwa kuandaa shughuli hiyo.
Alisema kuwa kuna baadhi ya vyama ambavyo vilitakiwa kushiriki lakini havijashiriki ambapo havijaathiri chochote na kuweka wazi kuwa wachache wanaweza kufanya mambo kwa ajili ya wengi.
"Kuna baadhi ya vyama havijashiriki maandamano haya, hivyo vikumbuke kuwa watu wachache wanaweza kufanya mambo kwa ajili ya wengi hivyo ni jambo kubwa na kwamba mungu analisikia,"alisema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya viongozi na wawalikishi wa vyama hivyo walisema kuwa watanzania wanapaswa kupiga kura kwa amani pia walishamaliza wakatulie nyumbani kusubiri matokeo kutoka kwa mawakala wanaowaamini waliowaweka vituoni.